Kituo cha Sheria na Utetezi wa Haki za
Binadamu (LHRC) na Chama Cha Wanasheria Tanzanyika vimefungua kesi ya
Kikatiba katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, vikiomba mahakama
hiyo itoe tafsiri za kisheria katika baadhi ya Ibara.
Kesi hiyo ya Kikatiba ambayo imepewa
namba 24 ya mwaka huu, na ambayo bado haijapangiwa jaji, wadaiwa ni
Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Taasisi hizo ambazo zinatetewa na
mawakili wa kujitegemea Harold Sungusia, Francis Stolla na wengine 17,
kwa mujibu wa hati yao ya madai, walalamikaji hao wamewasilisha jumla ya
maombi mawili ambayo wanaomba mahakama itoe tafsiri ya kisheria katika
Ibara hizo kwa kuwa wamewasilisha kesi hiyo ya Kikatiba chini ya sehemu
ya Tatu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977,
ambayo
inaainisha Haki na Wajibu Muhimu.
Wakili Sungusia alilitaja ombi la kwanza
kuwa, wanaiomba mahakama hiyo itamke kuwa ibara ya 100(1) ya Katiba ya
nchi inayotoa uhuru wa majadiliano kwa wabunge wawapo ndani ya bunge
ambayo inasomeka hivi: “kutakuwa na uhuru wa mawazo, majadiliano na
utaratibu katika Bunge na uhuru huo hautavunjwa wala kuhojiwa na chombo
chochote katika Jamhuri ya Muungano, au katikaMahakama au mahali
penginepo nje ya Bunge.”
Wakili Sungusia anadai kuwa Ibara hiyo
ina ubaguzi ndani yake kwani inayoa uhuru kwa mbunge kujadili ndani ya
bunge na wakati anajadili jambo hata kama amevunja haki za mtu mwingine
hataweza kushitakiwa wala kuhojiwa jambo ambalo anadai linakinzana na
Ibara ya 13(2) ya Katiba ambapo Ibara hii inasomeka hivi; “ Ni marufuku
kwa sheria yoyote iliyotungwa na mamlaka yoyote katika Jamhuri ya
Muungano kuweka sharti lolote ambalo ni la ubaguzi ama wa dhahiri au kwa
taathira yake’.
‘...sisi tunaomba mahakama itamke wazi
kuwa Ibara ya 100(1) inakwenda kinyume na matakwa ya Ibara 13(2).
Zinakinzana, kwa kuwa ibara ya 100(1) ya Katiba inatoa haki tu kwa
upande wa mmoja wa wabunge uhuru wao kutohojiwa na inawanyima haki ya
kuwahoji au kuwashitakiwa wabunge wanaotoa kauli zao bungeni hata kama
kauli hizo za wabunge zimevunja haki za wananchi,”alidai wakili
Sungusia.
Wakili Sungusia alilitaja dai la pili
kuwa ni kuiomba mahakama hiyo itamke kuwa kauli ya Waziri Mku, Pinda
ambayo ililitaka Jeshi la Polisi kuwapiga wale wote wanaokiuka amri za
jeshi hilo, kama kauli hiyo nayo inalindwa na kinga iliyowekwa katika
Ibara ya Ibara ya 100(2) ya Katiba ya nchi ambayo inasomeka hivi: ‘Bila
ya kuathiri Katiba hii au masharti ya sheria nyingine yoyote
inayohusika, Mbunge yeyote hatashtakiwa au kufunguliwa shauri la madai
mahakamani kutokana na jambo lolote alilolisema au kulifanya ndani ya
Bunge au alilolileta Bungeni kwa njia ya maombi, muswada, hoja au
vinginevyo.’
Katiba mkutano wa bunge uliomalizika
hivi karibuni , Waziri Mkuu Pinda akiwa ndani ya bunge aliliagiza jeshi
la polisi kuwapiga wale wote wanaokaidi amri za jeshi hilo, kwasababu
serikali imeshachoshwa na vitendo vya baadhi ya wananchi wanaokaidi kwa
makusudi amri za jeshi la polisi , kauli iliyoleta mhemko kwa jamii huku
wengine wakiipinga utekelezaji wa agizo hilo na wengine wakiunga mkono,
hali iliyosababisha LHRC hivi karibuni ilizungumza na waandishi wa
habari wakimtaka Pinda afute kauli yake hiyo ama sivyo watamfikisha
mahakamani.