Na Imelda Mtema
MOJA kati ya sifa kubwa ya mwanamke ni
kujua kupika. Zipo baadhi ya ndoa ambazo huvunjika kutokana na tatizo la
mwanamke kutojua kupika.
Kwenye ulimwengu wa mastaa wa kike Bongo, wapo wengi wanaojua kupika chakula kizuri na wapo ambao hawajui.
Kizuri huwa kinajiuza siku zote, sifa
njema huwa inazungumzwa na wengi ndiyo maana ni rahisi kuwasikia hata
wakisifiana wenyewe kwa wenyewe pindi wanapobaini miongoni mwao yupo
anayejua kupika zaidi.
Tathmini yangu ya kina katika safari
zangu za kila siku kwenye tasnia ya habari, nimeweza kujifunza kuwa wapo
mastaa ambao ni hodari kwa kupika na sifa zao zimekuwa zikikua siku
hadi siku.
Mara kadhaa nimeshawahi kuwasikia mastaa
wa kiume kama Jacob Steven ‘JB’, Vincet Kigosi ‘Ray’ Single Mtambalike
‘Richie’ wakiwasifia baadhi ya wasanii wa kike ambao wanajua kupika
vizuri.
Katika makala haya nakuletea baadhi ya
mastaa ambao wanaongoza kwa kutajwa kuwa ni ‘mafundi’ wa kupika
madikodiko ambapo kila mmoja ana siri yake iliyomfanya awe anajua
kukaangiza:
Aunty Ezekiel
Huyu ni staa ambaye kwa muonekano wa nje
anaonekana ni sistaduu anayejipenda sana na ukadhani si mtu wa kuingia
jikoni au kujishughulisha na kazi zozote za nyumbani, lakini ni mtaalam
wa kupika balaa.
Mwenyewe anasema alikuwa akipenda kupika
tangu akiwa mdogo na alikuwa hodari wa kuwaangalia watu aliokuwa
akiishi nao na kuweza kupata ujuzi wa mapishi. Ni mtaalam wa kupika
chakula chochote na ukibahatika kula utadhani kimepikwa kwenye mahoteli
yenye hadhi.
WEMA SEPETU
Beautiful Onyinye, Wema Sepetu ‘Madam’
ni hatari ukimkuta jikoni, anapokuwa jikoni siyo yule unayemuona kila
kukicha kwenye matukio mbalimbali, anapika vyakula ambayo mara nyingi
huwa ni vigumu kwa wanawake wengi kama katles, kababu, Sambusa na
vyakula vingine vingi.
Wema anasema ufundi wa jikoni aliupata
kutoka kwa mama yake mzazi, Mariam ambaye mara nyingi anapata tenda
kubwa za kupika vyakula sehemu mbalimbali hivyo alikuwa makini sana
kuiba ujuzi wake.
MONALISA
Yvonne Cherry ni msanii wa kitambo. Siku
moja nilipata bahati ya kwenda nyumbani kwao, Yombo Buza ambapo
nilimkuta akiwa jikoni na alipomaliza na kukionja chakula chake
nilikubali, anajua kuchanganya vitu vingi kwenye chakula na kuleta ladha
ya aina yake.
Monalisa anasema kuwa ufundi huo
aliupata kutoka kwa bibi yake, mama Ngatwika aliyekuwa akimfundisha
namna ya kupika vyakula mbalimbali.
JACQUELINE WOLPER
Yeye huwezi kujua kabisa kama ni mtaalam
wa jikoni. Ukibahatika kumkuta jikoni basi utagundua huwa anatumia muda
mwingi kuandaa chakula kitamu ndiyo maana baadhi ya wasanii wenzake
wanapenda kumpigia simu na kumwambia wanakwenda kula nyumbani kwake.
Wolper anasema kuwa utaalam wa jikoni
aliupata toka kwa mama yake kwani nyumbani kwao watoto wote bila kujali
jinsi wanafundishwa kupika.
JOHARI
Blandina Chagula ndiyo funga kazi. Ni
mtaalam balaa wa mapochopocho yote ambapo wasanii wenzake akiwemo Irene
Uwoya siku zote huwa anampigia ‘saluti’ na hata zinapotokea sherehe
ndogondogo yeye ndiyo hupewa nafasi ya kuwa msimazi wa kupika.
Mwenyewe anasema ujuzi huo ni kipaji
alichozaliwa nacho kwani toka akiwa mdogo, alikuwa na uwezo wa kupika
chakula cha kula watu wa nyumba nzima na kila mmoja akaridhika.