Wakati suala la ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki(EAC) likiendelea kujadiliwa namna ya utekelezaji wa mambo mbalimbali ikiwamo sarafu moja na suala la kisiasa, Baraza la Elimu ya Vyuo Vikuu kwa ukanda huu(IUCEA) linataka taasisi zake zitoe elimu inayofanana.
Msukumo wa kutoa kiwango cha elimu kinachofanana, unatokana na hali
iliyopo sasa kwa wahitimu wa vyuo vikuu katika nchi za EAC kushindwa
kumudu ushindani wa soko la ajira duniani.
Katibu Mtendaji wa IUCEA, Profesa Mayunga Nkunya anasema mfumo huo
utasaidia wahitimu wa jumuiya hiyo kupata taaluma itakayokuza mahitaji
katika soko la ajira duniani.
Akizungumzia mfumo wa elimu wa Tanzania, Profesa Nkunya anasema ni
wa kizamani ambao haimsaidii mwanafunzi anapohitimu masomo yake.
“Kwetu sisi mtihani ndiyo kigezo pekee cha kumpima mwanafunzi,
kufanya hivyo ni kosa kwa sababu kunawengine wanafeli lakini wanauwezo
mzuri tu kwenye masuala mengine. Tunataka kuwa na mfumo katika Afrika
Mashariki unaoangalia uwezo wa kila mtu” anasema.
Anasema kama nchi hizo zitaendelea na mfumo wa sasa wa kuchukulia
mtihani kuwa kipimo pekee cha kupima uelewa wa mwanafunzi, zitazidi
kupoteza nafasi nyingi za watu wenye uwezo.
Profesa huyo anasema katika nchi za EAC ni Rwanda pekee ndiyo
imebadili mfumo wake wa elimu ambao unatoa fursa kwa kila mtu kupata
elimu bila kuhukumiwa na kigezo cha kufaulu au kutokufaulu kwenye
mitihani.
Anaongeza kuwa nchi zilizoendelea duniani zimefanikiwa kutoa elimu
kwa watu wake kwa sababu kwao mitihani siyo kigezo cha kupima uwezo wa
mtu.
Akizungumzia mpango huo wa IUCEA Msemaji wa Tume ya Vyuo Vikuu hapa
nchini (TCU), Edward Mkaku anasema haoni ubaya wowote wa mpango huo
lakini IUCEA haina mamlaka katika vyuo vikuu vya Afrika Mashariki kwani
kila nchi ina sheria zake katika suala la elimu.
Mkaku anasema ili hatua hiyo ifikiwe, inabidi kila nchi mwanachama wa EAC iafiki kujiunga na mpango.
Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Biashara la Afrika Mashariki
(EABC), Andrew Kaggwa anasema anasema wahitimu wa elimu ya vyuo vikuu
katika nchi za EAC, wana ujuzi mdogo ambao hauwezi kufanya vizuri kwenye
soko la ushindani.
Kaggwa anasema mfumo huo wa elimu utasaidia EAC kutatua changamoto
ya ajira kwa wahitimu wa elimu ya juu kutokana na kile alichoeleza
kwamba wataweza kutengeneza bidhaa zao wenyewe badala ya kutegemea
bidhaa kutoka nje. Mkurugenzi huyo anasema wataalamu kutoka Asia, China
na Amerika ndiyo wamejaa katika nchi za EAC kwa sababu watu wa jumuiya
hii wamekosa ujuzi unaowasaidia kumudu kuendesha viwanda na biashara
katika nchi zao.
“Sisi tunawafanyia kazi wenzetu kwa kuwauzia malighafi ambazo wanazileta huku kama bidhaa na kutuuzia tena” anasema Kaggwa.
Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) mkoani
Morogoro, Eliaza Mkuna ambaye anasomea Shahada ya Uzamili wa Sayansi
katika Kilimo na Uchumi, anasema licha ya mpango huo kuwa mzuri, tatizo
lipo kwenye elimu ya chini.
“Jinsi tunavyomuandaa mwanafunzi kuanzia ngazi ya chini
tunatofautina katika nchi hizi tano, ukizingatia Tanzania tumekumbwa na
anguko la elimu kwa siku za hivi karibuni” anasema msomi huyo.
Anasema kuwa maandalizi ya kutosha yanahitajika kabla ya mpango huo
kuanza kazi. Anasema maono ya kielimu katika nchi hizi yanatofautiana
kutokana na kila moja kuwa na vipaumbele vyake.
“Tanzania tuna ‘Big Result Now’ je tunajua nchi nyingine zina dira gani? Je zinashabihiana?” anahoji Mkuna.
Anasema elimu inategemea vitu vingi ambavyo vinatofautiana kati ya
nchi moja na nyingine ambapo anatolea mfano wa vitabu vinavyotumika
kufundishia katika shule za Kenya ni tofauti na vile vinavyotumika
nchini Tanzania.
Jarida la IUCEA la mwaka jana lilimnukuu Rais wa Rwanda, Paul
Kagame akisema bado nchi za jumuiya ya Afrika Mashariki hazijafikia
lengo la Umoja wa Mataifa(UN) la kuwa na angalau asilimia 10 ya watu
wenye elimu ya kiwango cha chuo kikuu.
Rais Kagame anasema kiwango kilichopo sasa cha asilimia tano hadi saba ni kidogo ukilinganisha na lengo la UN.
Kagame anawataka viongozi wa IUCEA kutekeleza mipango yao ya
maendeleo na kuhakikisha kuwa vyuo vikuu vya EAC, vinashirikiana katika
rasilimali walizonazo ili kufanikiwa kitaaluma na kitafiti.
Kagame aliongeza kuwa nchi yake na wanachama wengine wa EAC
wanatarajia mipango yenye mashiko inayoakisi mafanikio ya kuwa na
jumuiya ya Afrika Mashariki.
Katika kuhakikisha mchakato huo unatimia Kaggwa anasema, baraza
hilo ambalo baadhi ya vipaumbele vyake ni pamoja na masuala ya weledi,
uwajibikaji, usawa na ubunifu limeandaa kongamano litakolishirikisha
wafanyabiashara, wataalamu na taasisi mbalimbali litakalofanyika jijini
Nairobi mwezi Oktoba mwaka huu. Lengo la kongamano hilo litakuwa ni
kukutanisha sekta za umma na binafsi ili kujadili namna ya kuboresha
sekta ya elimu katika nchi za EAC.
Baraza hilo linalenga kuunda mtandao wa vyuo vikuu kwa nchi za
ukanda wa Afrika Mashariki pamoja na vya nje ya jumuiya hiyo. Pia
linalengo la kuunda jukwaa litakalokuwa linajadili masuala ya kitaaluma
na mambo mengine yanayohusiana na elimu ya juu.