JINA la Aunt Ezekiel siyo geni kabisa kwa wadau mbalimbali wa burudani
hapa nchini, ni staa ambaye hivi sasa ana jina kubwa kupitia sanaa yake
ya uigizaji wa filamu aliyoianza miaka sita iliyopita.
Japokuwa kwa sasa ni staa, amepitia mambo mengi magumu katika safari yake ya maisha mpaka kufikia hapo alipo hivi sasa.Aunt alizaliwa mwaka 1988 mkoani Dar es Salaam, baba yake akijulikana kama Ezekiel Grayson’ Jujuman’ ambaye alikuwa ni mchezaji hodari sana wa timu ya Simba. Alipata elimu yake ya msingi katika Shule ya Bunge mwaka 1993 hadi 1998. Alienda kumalizia darasa la saba katika Shule ya Msingi Chanzige iliyopo Kisarawe, mkoani Pwani.
Vipi maisha yalikuwaje baada ya kumaliza shule?
“Kwa kweli maisha yalikuwa ni magumu mno kwa maana nilipomaliza shule tu, alijitokeza mwanaume na kutaka kunioa kitu ambacho mimi sikukipenda kabisa lakini baba yangu alitaka hivyo kwa vile uwezo wa kunisomesha hakuwa nao tena na maisha yalikuwa ni magumu sana.