HATIMAYE ripoti ya Tume ya Haki za
Binadamu na Utawala Bora, kuhusu vitendo vya uvunjaji wa haki za
binadamu na mauaji yaliyotokea Arusha Januari 5, 2011 kwenye maandamano
ya CHADEMA imevuja.
Licha ya ripoti hiyo kufichwa kwa
kutosomwa hadharani kwenye vyombo vya habari kutokana na kulishutumu
moja kwa moja Jeshi la Polisi, Tanzania Daima imefanikiwa kuinasa.
Maandamano hayo ya CHADEMA ya kupinga
ukiukwaji wa kanuni na sheria katika uchaguzi wa Meya ya Manispaa ya
Arusha, Gaudence Lyimo, licha ya kuruhusiwa na polisi awali baadaye
yalipigwa marufuku na Mkuu wa Jeshi hilo nchini, IGP Saidi Mwema.
Hata hivyo, CHADEMA walikataa kutii
agizo hilo kutokana na taarifa ya IGP kutowafikia kwa maandishi kama
inavyoelekezwa kwa mujibu wa taratibu za utendaji wa jeshi hilo.
Kufuatia vurugu hizo za polisi na
wafuasi wa CHADEMA, watu watatu waliuawa kwa kupigwa risasi, wengine
zaidi yya 30 kujeruhiwa na wafuasi zaidi ya 70 wakiwemo viongozi
waandamizi wa chama ambao walifunguliwa mashtaka mahakamani.
Kutokana na tukio hilo Tume ya Haki za
Binadamu, iliunda tume iliyochunguza suala hilo Januari 10 hadi 13 mwaka
2011, kwa kuwahoji viongozi wa CHADEMA mkoa wa Arusha, Jeshi la Polisi,
hospitalini walipolazwa majeruhi na njiani walipoandamana wafuasi wa
chama hicho.
Tume hiyo iliongozwa na Kamishna
Joaquine De-Mello akiandamana na ofisa uchunguzi, Philipo Sungu, kutoka
idara ya elimu kwa umma na mafunzo kufuatilia tukio hilo kwa muda wa
siku tatu ili kupata picha halisi.
Lengo kuu lilikuwa kubaini chanzo cha
vurugu hiyo, uvunjwaji wa haki za binadamu ambapo Januari 11, asubuhi
tume hiyo ilianza kuonana na madaktari na wagonjwa majeruhi waliolazwa
katika hospitali mbili za Mount Meru na Seliani.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo ambayo gazeti
hili linayo nakala yake, taarifa zilizopatikana katika hospitali
zilionyesha kupokelewa kwa majeruhi 26 katika hospitali ya Mount Meru na
wawili Seliani.
Majeruhi watatu walipoteza maisha wakati
wakipatiwa matibabu ya awali hapo hospitali ya Mount Meru, 22 walilazwa
katika hospitali ya Mount Meru na watatu walipatiwa matibabu na
kuruhusiwa kuondoka hospitalini.
Ripoti ya madaktari ilithibitisha kuwa
vifo hivyo vilitokana na majeraha ya risasi za moto huku majeruhi
wengine wakithibitisha kupigwa risasi za moto huku wakionyesha majeraha
hayo kwenye miili yao.
Licha ya ripoti kuonyesha vitendo hivyo
vya uvunjifu wa haki za binadamu uliofanywa na polisi, inasema kuwa
maandamano ya CHADEMA na mkutano yalikuwa halali na jeshi ndilo
lilisababisha fujo hizo kwa kutofuata sheria.
“Tanzania inajivunia Katiba inayoainisha
vipengele mbalimbali vinavyotambua na kulinda haki za msingi za
binadamu, hivyo kama nchi nyingine inawajibika kwa Azimio la Ulimwengu
la Haki za Binadamu la mwaka 1948 (UDHR) ambalo ni mama wa matamko,
makubaliano na mikataba ya vizazi vyote vya haki,” inasema ripoti hiyo.
Kwamba Tanzania kama miongoni mwa nchi
wanachama zilizoweka sahihi na kuridhia mikataba hiyo zinawajibika moja
kwa moja “kuheshimu, kulinda, kutetea na kutekeleza” haki zilizoainishwa
kwenye mikataba husika.
Ripoti hiyo inaongeza kuwa “kanuni za
jumla za jeshi la polisi namba 403 kifungu cha kwanza inasema; Mtu
yeyote ambaye anataka kuitisha, kukusanya, kuandaa na mkutano wowote au
maandamano katika eneo lolote hadharani atapaswa kuwasilisha taarifa ya
maandishi si chini ya saa 48 kabla ya wakati mkutano au maandamano
kufanyika kwa ofisa wa polisi wa wilaya husika.
Na pindi anapopelekea taarifa kwa
maandishi kwa mkuu wa polisi wa wilaya anaruhusiwa kuendelea kuandaa,
kuitisha, kukusanya, kuunda, au kuandaa mkutano au maandamano kama
ilivyopangwa.
Ila mpaka atakapopata taarifa ya
maandishi kutoka kwa Afisa Polisi wa Wilaya husika kueleza sababu za
kusitisha maandamano hayo.”
Ripoti hiyo inasema kuwa kwa mujibu wa
sheria hiyo, polisi “Officer in charge” wa eneo katika eneo hilo la
Arusha mjini ni OCD wa Arusha Mjini – ndiye aliyepaswa kutoa maelekezo
ya kuzuia maandamano na si Kamanda wa Polisi wa Mkoa au Inspekta
Jenerali wa Polisi.
“Kwa mantiki hii, taarifa ya CHADEMA kwa
polisi ilitosha kwa wao kuendelea na mipango yao ya maandamano na
mkutano kama inavyoelezwa kisheria,” anasomeka taarifa hiyo.
Pia inaonyesha kuwa Sheria Na. tano (5)
ya mwaka 1992 ya vyama vya siasa kifungu cha 11 vifungu vidogo vya (4)
na (6) na sheria Na. 1 ya 1939 ya polisi na huduma za mgambo kifungu
43.-(1), (2), zilikidhi pia hitaji la CHADEMA kuendelea na mipango yao
ya maandamano na mkutano wa hadhara kama ilivyopangwa.
Kwamba Sheria Na.5, 1992 ya vyama vya
siasa kifungu 11. — (8) inasema: kama jeshi la polisi linasitisha
maandamano au mkutano taarifa hizo hutolewa kwa maandishi kueleza
sababu, wala si kutumia televisheni, kama ilivyojitokeza kwa tukio la
Arusha.
“Hivyo CHADEMA walikuwa sahihi kwa kuwa
hawakupata taarifa ya kimaandishi licha ya polisi kudai kutoa barua hiyo
lakini walishindwa kuthibitisha madai yao mbele ya tume.
Ripoti hiyo pia inaongeza kuwa askari
walifanya vitendo vya unyanyasaji na udhalilishaji dhidi ya viongozi na
waandamanaji hasa wanawake bila kujali hali zao.
Kwa mfano wanatajwa mbunge wa viti
maalum Lucy Owenya na mke wa Katibu Mkuu wa CHADEMA, Josephine
Mushumbusi, kuwa walipigwa na kujeruhiwa vibaya sehemu mbalimbali za
miili yao.
Kwamba viongozi wa CHADEMA na wananchi wengi walikamatwa na kuwekwa rumande katika kituo kikuu cha polisi kati mjini Arusha.
“Askari waliwapiga waandishi wa habari,
waliwanyang’anya vifaa vyao vya kazi na kufuta picha na kazi walizokuwa
wanazifanya kwenye maandamano. Askari na waandamanaji walisababisha
uharibifu wa magari na mali za umma na wananchi.
“Aidha walisababisha upotevu wa mali za
wananchi zikiwemo simu mbili za mkononi za Owenya na fedha tasilimu sh
2,700,000 za majeruhi Ally Ogaga walizodai kunyang’anywa na askari,
wakati Ofisi ya CCM Mkoa wa Arusha ilivunjwa vioo kwa mawe na
waandamanaji na nyumba ya mwananchi Salum Ally iliungua kwa moto
uliosababishwa na mlipuko wa bomu lililoruka kutoka kwenye gari la
polisi,” ilisomeka.
Tanzania Daima