
MWANAFUNZI wa kidato cha kwanza katika shule ya sekondari Marangu 
inayomilikiwa na kanisa Katoliki jimbo la Moshi, (jina limehifadhiwa) 
alitekwa na kukufungiwa kwenye hoteli moja ya kitalii mjini hapa na 
kufanyiwa vitendo vya ngono kwa muda wa siku nne mfululizo.
Mwanafunzi huyo anadaiwa kutekwa Agosti 6 mwaka huu na kijana mmoja 
(jina linahifadhiwa) mfanyakazi wa kampuni ya simu za mikononi (Airtel) 
mjini Dodoma.
Akizungumza jana na Tanzania Daima Jumatano, kaka wa mwanafunzi huyo, 
Joseph Temba, alidai mdogo wake alitekwa na mtu huyo na tayari mtuhumiwa
 ameshakamatwa.
Alisema walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo Agosti 10, mwaka huu, 
katika baa moja akiwa na mdogo wake baada ya raia wema kutoa taarifa za 
kuonekana kwake.
Kwa mujibu wa kaka wa mwanfunzi huyo siku ya tukio alipokea simu kutoka 
kwa mwangalizi wa wanafunzi (matroni) akimjulisha kutokuwapo bwenini kwa
 mdogo wake na ndipo walipoanza kufuatilia na kutoa taarifa kituo kikuu 
cha polisi mjini Moshi na kupewa namba Mos/RB/9196/2013.
Alisema siku iliyofuata ya Agosti saba jioni walipokea simu kutoka kwa 
watu wa karibu wakiwataarifu kuwapo katika hoteli hiyo mdogo wake lakini
 baada ya kufika walinyimwa kuona kitabu cha wageni ili kuangalia orodha
 ya majina ya wageni waliofikia hapo ili kujiridhisha kama mtuhumiwa 
huyo alikuwapo mahali hapo.
Hata hivyo alisema jioni ya Agosti 10 walipokea taarifa za kuonekana 
kwenye baa hiyo mtuhumiwa akiwa na mdogo wake na kuwajulisha polisi na 
hatimaye kufanikiwa kumtia mbaroni ambapo hadi sasa bado anahojiwa na 
jeshi la polisi.
Chanzo cha kutekwa kwa mwanafunzi huyo ni mawasiliano ya simu baina ya 
mtekaji na mwanafunzi huyo ambapo inadaiwa mtuhumiwa huyo alimrubuni 
mwafunzi huyo kuacha masomo na kwamba angemtafutia nafasi kwenye shule 
kubwa za kimataifa.
Inadaiwa kwamba mwanfunzi huyo alikubaliana na propaganda hiyo na kutoka
 shuleni jioni ya Agosti 6 na kumfuata mtuhumiwa kwenye gari lake na 
kwenda naye hadi Moshi mjini umbali wa kilomteta 50 kutoka shule ya 
sekondari Marangu.
Kamanda wa polisi mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz, alisema hana taarifa
 za kutekwa kwa mwanafunzi huyo kwa kile alichodai alikuwa ametingwa na 
majukumu ya kikazi mjini Arusha na kuahidi kulifuatilia baadaye. 
Tanzania daima