IMEBAINIKA kuwa baadhi ya maofisa wa
polisi na makachero wao wamekuwa wanatumia vibaya majina ya viongozi
wakuu wa serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kama kisingizio cha
kupika kesi za ugaidi dhidi ya viongozi wakuu wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA).
Katika tukio la hivi karibuni, makada wa
CHADEMA waliokuwa rumande wakikabiliwa na mashitaka ya ugaidi, ambayo
hatimaye yalifutwa na mahakama, wametoboa siri kuwa miongoni mwa majina
yaliyotumiwa na baadhi ya polisi na makachero waliowatesa ni ya Rais
Jakaya Kikwete; na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto,
Sophia Simba.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati
tofauti, wiki hii, makada hao - Evodius Justinian, Oscar Kaijage, Rajabu
Kihawa, Seif Magesa na Henry Kileo, wamesema pia kuwa njama hizo za
polisi na makachero wao, zililenga kuwalazimisha vijana hao wawahusishe
viongozi wakuu wa CHADEMA (hasa Mwenyekiti, Freeman Mbowe na Katibu
Mkuu, Dk. Willibrod Slaa) na ugaidi na utesaji watu ambao umekuwa
unaendelea.
Wengine ambao polisi walitaka watajwe ni Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika.
Hata hivyo, vijana hao wanasema waligoma kuwahusisha, hata baada ya kuteswa kikatili.
Makada hao wanadai kwamba mateso waliyopata yaliratibiwa na viongozi wa Jeshi la Polisi, Advocate Nyombi na afande Pasua.
Mmoja wa makada hao, Kihawa,
aliyekamatwa na kupelekwa Kituo cha Polisi Dodoma, anadai kuwa alipokuwa
anahojiwa, alilazimishwa aseme kuwa viongozi wa CHADEMA ndio wanahusika
na utekaji na tindikali.
Akiendelea kusimulia mkasa huo, Kihawa
alisema kuwa baada ya kauli hiyo, aliingizwa katika chumba namba 114,
ghorofa ya pili, chenye kamera nyingi katika moja ya hoteli maarufu
Mjini Dodoma (jina tunalihifadhi kwa sasa) akavuliwa nguo zote,
akakalishwa kwenye chupa ya soda kisha akapigwa sana.
“Nilipoteza fahamu lakini nilipozinduka
nilikuta nimevalishwa nguo, na nimekalishwa kwenye kiti na kuwekewa
chakula karibu,” anasema, na kuongeza kuwa hakula chakula hicho, lakini
alipotoka nje ya chumba hicho, kwenye ukumbi wa hoteli, aliwakuta vijana
waliofukuzwa CHADEMA, Juliana Shonza na Mtela Mwampamba na Habib
Mchange wakinywa na kula.
“Walinikejeli sana, wakasema wanashangilia ushindi,” alisema.
Kutoka pale nilichukuliwa na Mbunge wa
Maswa Magharibi, John Shibuda, akaniingiza chumbani akadai anampigia
simu Waziri Simba, akamwambia, “mama, huyu kijana ninaye hapa. Ungeongea
naye ili akubali kulegeza msimamo, au umpigie mwanao Jakaya anipigie,
pengine atabadili msimamo wake kama tulivyokuwa tumekubaliana awali.”
Kihawa anadai kuwa mtu huyo aliyedaiwa
kuwa Waziri Simba alimjibu Shibuda kuwa asingeweza kuzungumza yeye kwa
kuwa alikuwa hajisikii vema, ila kwa suala la kuongea na Rais Kikwete,
atafutwe Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana au Naibu Katibu
Mkuu Bara, Mwigulu Nchemba, ili awaunganishe Shibuda na rais.
Kwa mujibu wa Kihawa, baada ya kupewa
ushauri huo, Shibuda alijibu: “Mwigulu ni mropokaji, hawezi kuingizwa
katika mkakati huu; na Kinana ni mgumu kuingilika katika suala hili.”
Anasema alisikia mazungumzo yao kwenye
loud speaker ya simu ya Shibuda, na baada ya kukata simu Shibuda
alimwambia kuwa alikuwa anazungumza na Simba, ambaye alidai ni ‘mama
mdogo wa Kikwete.’
Kihawa anasema wakati anahojiwa hayo hapo hotelini, maofisa wa polisi walisimama kwa mbali wakimsubiri.
Wengine waliokuwapo wakishuhudia
mahojiano hayo ni Meya wa Ilemela, Henry Matata na aliyekuwa Diwani wa
Igoma, Adam Chagulani. Matata na Chagulani walishavuliwa uanachama na
CHADEMA.
Wahusika walipohojiwa na Tanzania Daima jana, kila mmoja alikuwa na kauli yake kama ifuatavyo:
Tanzania Daima Jumapili: Afande Nyombi,
vijana waliokuwa wametuhumiwa kwa kesi ya ugaidi kule Tabora, wamekutaja
wewe kuwa ulishiriki kuwatesa ukiwalazimisha wawataje viongozi wakuu wa
CHADEMA kuwa walishiriki kutenda ugaidi na utekaji. Unatoa ufafanuzi
gani?
Advocate Nyombi: Mimi si msemaji wa Jeshi la Polisi, siwezi kusema chochote.
Tanzania Daima Jumapili: Msemaji
atajuaje kama mliwatesa watu wakati wa mahojiano? Mbona huku ni kumwonea
msemaji wa Jeshi la Polisi kusemea kila kitu hata mambo ambayo askari
fulani ametenda kwa utashi wake?
Advocate Nyombi: Nimekwambia mtafute, msemaji katika hayo yote. Mimi siwezi kuongelea suala hilo, nakutakia Idd Mubaraka njema.
Tanzania Daima Jumapili: Afande Pasua,
vijana waliotuhumiwa katika kesi ya ugaidi kule Tabora wamekutaja wewe
kuwa ulishiriki kuwatesa, ukiwalazimisha wataje viongozi wa CHADEMA kuwa
walishiriki kutenda ugaidi na utekaji. Unatoa ufafanuzi gani?
Afande Pasua: Kwani wewe uko wapi?
Tanzania Daima Jumapili: Nipo Dar es Salaam, hapa ofisini.
Afande Pasua: Njoo ofisini tuongee tuyaweke sawa unayouliza. Umesema unatoka gazeti gani?
Tanzania Daima Jumapili: Nimekwambia Tanzania Daima.
Afande Pasua: Mashtaka hayo kwanza
yalikuwa ya serikali, mimi sifanyi kazi ya kubahatisha, mpigie msemaji
wa Jeshi la Polisi mimi si msemaji. Alikata simu.
Henry Matata
Tanzania Daima Jumapili: Mstahiki Meya,
vijana waliokuwa wanakabiliwa na kesi ya ugaidi wanadai walihojiwa mbele
yako Dodoma. Je, unafahamu nini kuhusu suala hili?
Matata: Kijana Rajab Kihawa ndio
namfahamu. Huyu alikuwa mfanyakazi wangu, ila tangu aache kufanya kazi
hapa sijaonana naye. Lakini mimi nina ugomvi na wafanyakazi wote wa
gazeti lenu na gazeti lenu. Nisingependa kuongea na nyie. Tangu
nifukuzwe CHADEMA gazeti lenu linaongeza chumvi habari zinazonihusu.
Mimi si meya kwa kura za CHADEMA. CHADEMA walinifukuza, CCM wakaona
nafaa, wakanipa kura nikawa meya.
Tanzania Daima Jumapili: Ulikutana na Rajab Dodoma hotelini?
Matata: Nimekwambia sitaki kuongea na gazeti lenu.
bi Mheshimiwa, vijana waliokuwa
wanakabiliwa na kesi ya ugaidi wamekutaja kuwa ulikuwepo wakati
wanahojiwa Dodoma. Je, una kauli gani kwa yao hii?
Chagulani: Mimi nilikuwa Dodoma mwezi wa
nne lakini nilikuwa Kondoa kwa ajili ya uhamisho wa mke wangu. Hayo
unayonieleza siyajui.
Waziri Simba hakupokea simu, na alipotumiwa ujumbe mfupi wa simu hakujibu lolote.
Msemaji wa jeshi la Polisi, Advera
Senso, alipoulizwa kama jeshi ndilo linawatuma polisi kutesa watu wakati
linawahoji, alisema: “Mhalifu asitafute huruma ya jamii kwa kuzushia
jeshi kwa uhalifu alioutenda yeye, na endapo ikibainika anasingizia
uongo na hilo ni kosa pia, kwani Jeshi la Polisi linafuata taratibu za
sheria.”
Shibuda alipoulizwa jinsi alivyohusika
katika sakata hilo alisema kuwa kwa sasa hawezi kuzungumza chochote kwa
kuwa alikuwa Agha Khan Hospitali akihangaikia mgonjwa wake.
“Niacheni kwa sasa kwa kuwa nahitaji
utulivu wa akili niweze kushughulikia afya ya mgonjwa wangu. Nadhani
hata kama ni wewe sijui katika mazingira kama haya ungeweza kweli
kuongea?” alisema.
Msemaji wa Ikulu, Salva Rweyemamu,
alipopigiwa simu kuulizwa ikiwa wanayo taarifa ya watu wanaotumia vibaya
jina la rais katika matukio ya kihalifu aliomba jambo lolote
linalohusiana na kazi, lisubiri kwa kuwa alikuwa katika mapumziko ya
sikukuu.
“Ndugu yangu, unajua leo ni sikukuu na
ni usiku, nitafute wakati mwingine, maana siwezi kuzungumzia mambo ya
watu wa CHADEMA muda huu. Niache nipumzike kidogo halafu tuwasiliane
siku ya kazi,” alisema