Serikali ya Rwanda imetoa tamko
linaloonyesha kutoielewa kauli ya Rais Jakaya Kikwete, iliyoamuru
wahamiaji haramu kuondoka nchini, hali inayoonekana kukwepesha hoja.
Rwanda kupitia waziri wake wa Mambo ya
Nje, Louise Mushikiwabo, ilikaririwa ikieleza kwamba hawatajibu mapigo
agizo la Rais Jakaya Kikwete ya kuwataka Wanyarwanda wote waliolowea
Magharibi mwa Tanzania kuondoka haraka.
Mushikiwabo alisema wako tayari
kuwapokea na kuwalinda wote waliofukuzwa Tanzania kwa kisingizio kuwa ni
wahamiaji haramu, akieleza kwamba anasikitishwa kwa kuwa Tanzania
haikufanya jitihada yoyote kuwasiliana na Rwanda kuhusu suala hilo kabla
ya kuchukua uamuzi huo.
“Ni uamuzi ambao umeshachukuliwa,
hatukushirikishwa kwa namna yoyote na jukumu letu kama serikali na taifa
ni kuwahakikishia ulinzi wote wanaokuja, na hili ndilo suala
tunalolishughulikia kwa sasa,” alisema.
Kwa mujibu wa gazeti la New Times,
Mushikiwabo aliwaeleza waandishi wa habari kwamba agizo hilo la Rais
Kikwete pamoja na ushauri wa kuitaka Serikali ya Rwanda kuzungumza na
wanamgambo hasimu wa FDLR waliopo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
(DRC), hayatayumbisha uhusiano imara baina ya Watanzania na Wanyarwanda.
“Sisi si majirani tu, tuna mfungamano
imara baina ya watu wetu pia, tuna mfungamano wa damu, wa kibiashara, na
mengine mengi ya kutufanya tuendelee kuwa pamoja,” alisema na kutumia
fursa hiyo kuwakaribisha Watanzania nchini Rwanda.
Watanzania wanaweza kuishi hapa kwa umri
wowote wanaotaka. Tunawachukulia kuwa ni watu wetu muhimu kwenye
fungamano la Jumuiya ya Afrika Mashariki,” alisisitiza.
Rais Kikwete wakati akihitimisha ziara
yake mkoani Kagera alitoa agizo la kuwataka wanaomiliki silaha kinyume
cha sheria na wahamiaji haramu ama kuondoka au kuhalalisha ukazi wao,
huku akitoa wiki mbili kwa zoezi hilo kutekelezwa, kabla ya kuanza kwa
operesheni ya kuwasaka watu hao.
Kauli hiyo ilitokana na kushamiri
vitendo vya kihalifu katika eneo la Kanda ya Ziwa, Rais hakutaja jina la
nchi ya wahamiaji hao. Kwa ukanda huo Tanzania inapakana na Kenya,
Uganda, Rwanda, Burundi na DRC.
Pia, Rais Kikwete katika hotuba yake ya
mwisho wa mwezi alizungumzia kusikitishwa na kauli za shutuma, kejeli na
udhalilishaji zilizotolewa na Rais Paul Kagame wa Rwanda dhidi yake.
Mvutano baina ya Rwanda na Tanzania
ulianza kuwekwa hadharani Mei mwaka huu, baada ya Rais Kikwete kuishauri
Rwanda kukaa na kuzungumza na FDLR wenye makao yao DRC, hatua ambayo
haikuifurahisha Serikali ya Rwanda.
Wakati Rwanda ikieleza hayo jana Katibu
Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue alizungumza na gazeti hili, na kutaka majibu
ya kauli hiyo ya Rwanda yatolewe na Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje,
Mkumbwa Ally alisema kauli iliyotolewa na Rais Kikwete ilikuwa ni
ushauri, kwamba Rwanda wanaweza kuukubali ama la.
“Kilichomkasirisha Rais Kikwete ni lugha
za matusi zilizokuwa zikitolewa na viongozi wa Rwanda, ila kwa hicho
walichokisema sidhani kama kitakuwa na tatizo kwetu,” alisema Mkumbwa.
Alifafanua kwamba, alipokuwa mkoani
Kagera Rais Kikwete hakutoa agizo la Wanyarwanda kufukuzwa, bali alitoa
agizo la kuanza kwa operesheni ya kuwakamata wahamiaji haramu, wale
wanaomiliki silaha kinyume na taratibu.
“Rais alizungumzia masuala ya jinai ‘Criminal Element’, siyo kuwafukuza Wanyarwanda,” alisisitiza.
Hatutazungumza na FDLR
Waziri wa Mambo ya Nje, Louise
Mushikiwabo, aliendelea kusema sera ya Rwanda kuhusiana na makundi ya
aina hiyo, iko wazi na haitabadilika, kauli ambayo amekuwa akiirudia
kila mara na kuwataka wote wanaofikiria kuhusu Rwanda kuzungumza na FDLR
kwa namna yoyote kusahau wazo hilo.
“Kama umehusika kwa namna yoyote na
maangamizi, wewe utakuwa adui wa kila mtu. Ni wazi kwamba Wanyarwanda
wote watakuwa kwenye majonzi iwapo kwa namna yoyote kutakuwa na
mawasiliano ya FDLR,” alifafanua.
Kundi la FDLR ambalo ni kifupisho cha
Democratic Forces for the Liberation of Rwanda, linaundwa na watu
walioshiriki kwenye mauaji ya kimbari yaliyowalenga watu wa kabila la
Watutsi mwaka 1994, na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 800,000 kwa
miezi mitatu.
Kundi hilo ambalo limeweka makazi yake
mashariki mwa DRC, linadaiwa kufanya mashambulizi kadhaa yakiwamo ya
milipuko ya mabomu nchini Rwanda, ambapo mwezi uliopita shambulio la
aina hiyo mjini Kigali lilisababisha vifo vya watu watatu na kujeruhi
watu kadhaa.
Uhusiano wa kihistoria
Familia za Rwanda zikiwamo zilizoishi
Tanzania tangu miaka ya 1950, zimeelezwa kuwa zimekuwa zikiwasili nchini
humo kupitia mpaka wa Rusumo baada ya agizo la Rais Kikwete kuwataka
wawe wameondoka ndani ya wiki mbili, kabla ya kuanza kwa operesheni
rasmi ya kuwaondoa.
Kwa mujibu wa mamlaka nchini Rwanda,
mamia ya Wanyarwanda waliokuwa wakiishi mkoani Kagera ambako ndiko
Tanzania inapopakana na Rwanda wamekuwa wakirejea kwa wingi, ambapo hadi
juzi, zaidi ya watu 300 walikuwa wameshaorodheshwa kwenye ofisi za
Uhamiaji.
-Mwananchi